Na
Juhudi Felix
KARAGWE
Wilaya ya Karagwe inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi kuanzia
ngazi za vijiji hadi wilaya hali inayopelekea kukwamisha shughuli za utoaji
huduma kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya
Karagwe Dary Ibrahimu Rwegasira katika
kikao cha Baraza la madiwani
kilichofanyika jana kwenye ukumbi
wa kituo rafiki cha Vijana maarufu kama
angaza kilichopo mjini Kayanga wilayani
hapa.
Alisema kuwa wilaya inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
upungufu wa watumishi kuanzia ngazi ya vijiji,kata na wilaya hali inayosababisha kukwamisha utoaji huduma
kwa uhakika na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.
Rwegasira alisema kuwa changamoto nyingine zinazoikabili wilaya ya
karagwe ni ugonjwa wa mnyauko wa migomba
na ukame ambazo zimeathiri sana maendeleo ya wilaya kwani wananchi
na wenyeji wa Karagwe hutegemea kilimo cha migomba na mazao mbalimbali
ya chakula hivyo ukame umeathiri sana
shughuli za kilimo.
Aidha,alibainisha kuwa vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji
kwa mwaka 2013 vimeongezeka tofauti
na miaka mingine ni kutokana na
kutokuwepo ushirikiano wa wahusika na vyombo vya dola.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya
amewataka wananchi kudumisha uzalendo kwa nchi yao na haswa katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi wa serikali za
mitaa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment